Tuesday, September 7, 2010

01

01

Tao inayoweza kuelezewa siyo Tao ya milele.
Jina linaloweza kutajwa kama jina sio jina la milele.

Kisichowezekana kupewa jina ndicho kilicho milele, cha kweli.
Kupewa jina ndio mwanzo wa vitu vyote vilivyopo ulimwenguni.


Huru kutokana na matamanio
huigundua ajabu hii.
Ukidakwa na matamanio basi utakachokiona ni vitu vinavyoonekana kwa nje tu.

Lakini ajabu na dalili za kuwepo ni vitu vinavyoanzia kwenye chanzo kimoja.
Chanzo hicho huitwa giza.

Giza ndani ya giza,
lango kuu kuingia kwenye uelewa wa kila jambo.

AYA ZA MTAWA
[ Tao-Te-Ching ]

02

Wakati watu wanapoona baadhi ya vitu kama vinavyopendeza;
vitu vingine huonekana vinavyochukiza na vibaya.
Watu wanapoona vitu vingine ni vizuri,
basi vingine hugeuka vyenye sura mbaya.

Kuwa na kuwepo ni vitu viwili vinavyoumbana;
Ugumu na urahisi wa mambo ni vitu vinavyoungana mkono;
Refu na fupi hufafanuana;
Juu na chini hutegemeana;
Kabla na baadaye hufuatana.

Kwa hiyo mwalimu hufanza bila kufanya kitu chochote
na hufundisha bila kusema chochote.
Vitu huzuka na huviachia vije,
Vitu hutoweka na huviachia kwenda zake.
Huwa navyo lakini hamiliki,
hufanya mambo bila kutarajia chochote.
Na kazi yake ikishafanyika huisahau.
Ndio sababu kazi zake hudumu milele.


AYA ZA MTAWA
[ Tao-Te-Ching ]

03

03
Ukiwaheshimu watu wakubwa kupita kiasi au kupindukia,
Watu hukosa nguvu na uwezo.

Ukizipa mali thamani kuliko watu,
basi watu huanza kuiba na kuwa wezi.

Mwalimu huongoza kwa kupakua kwanza akili za watu zikabakia tupu,
na kisha huanza kujaza akilini
kwa kudhibiti matamanio yao na kuamsha utu, ubinadamu na hamasa zao.
Huwasaidia watu kupoteza kila kitu wanachojua, wanachokitamani na kuzusha kuchanganyikiwa miongoni mwa wale wanaodhani wanajua.

Anza kufanya mazoezi ya kutofanya kitu chochote na kila kitu kitajiendesha chenyewe kwa asili bila kasoro.

AYA ZA MTAWA
[ Tao-Te-Ching ]

04

Tao ni kama kisima cha maji,
Watu hukitumia, lakini watu hawachoti maji kikaisha;
Ni kama anga tupu tusiyoiona ambayo kumbe imejaa kila aina ya vitu.

Imejificha lakini siku zote ipo.
Sijui ni nani aliyeizaa,
lakini hakuna anayeishinda kwa umri !

AYA ZA MTAWA
[ Tao-Te-Ching ]

05

Tao haifungamani na upande wowote,
Huzaa wema na wabaya,
Mwalimu naye hafungamani na yeyote,
huwakaribisha wote,
watukufu na wenye dhambi.

Tao ni kama kiriba:
kwa kawaida ni kitupu lakini kina uwezo wa kufanya kazi kubwa.
Kadri unavyoitumia ndivyo inavyofanya kazi zaidi.
Kadri unavyoizungumzia ndivyo unavyozidi kutoielewa zaidi.

Kaa na shilkilia papo hapo katikati .

AYA ZA MTAWA
[ Tao-Te-Ching ]

06

Tao huitwa Mama Mkuu,
tupu lakini isiyomalizika,
huzaa dunia kadhaa zisizo na idadi.

Sikuzote iko ndani yako,
na unaweza kuitumia kwa namna yoyote utakayo.

AYA ZA MTAWA
[ Tao-Te-Ching ]

07

Tao haihesebaki, haina idadi na ni isiyo na mwisho.
Kwanini haina mwisho na haifi ?
Haina mwisho na haifi kwa sababu haikuzaliwa;
kwa hiyo haiwezi ikafa.
Kwanini haihesabiki ?
Haina matamanio ya kujinufaisha yenyewe;
Kwa hiyo ipo kwa ajili ya kila kiumbe duniani.

Mwalimu siku zote hubakia nyuma;
Na ndio sababu siku zote yuko mbele ya wengine.
Hujitenga na vitu vyote;
Na ndio sababu yeye na hivyo vitu vingine ni kitu kimoja.
Kwa sababu amejiachia kwa vitu vyote,
huwa hana anachokikosa.

AYA ZA MTAWA
[ Tao-Te-Ching ]